DIR Return Create A Forum - Home
---------------------------------------------------------
habari
HTML https://habari.createaforum.com
---------------------------------------------------------
*****************************************************
DIR Return to: Jukwaa la elimu Tanzania
*****************************************************
#Post#: 1391--------------------------------------------------
SHULE BORA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2014
DIR By: mando
Date: February 15, 2015, 9:52 am
---------------------------------------------------------
SHULE BINAFSI ZATESA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE
HTML http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/2624432/highRes/945935/-/maxw/600/-/beu9utz/-/bora.jpg
Ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne umeongezeka
kwa asilimia 10, chini kidogo ya viwango vya Matokeo Makubwa
Sasa (BRN), lakini shule za Serikali za vipaji maalumu, kongwe
na za seminari zimeendelea kuporomoka. Katika matokeo hayo,
Shule ya Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera, iliyoanzishwa
mwaka 2010, ndiyo imekuwa kinara ikiwa ni mwendelezo wa
mafanikio baada ya mwaka jana kushika nafasi hiyo lakini kwa
upande wa shule zenye watahiniwa chini ya 40. Shule iliyoshika
mkia ni Manolo iliyopo Tanga, mkoa ambao umetoa shule tano
miongoni mwa shule zilizoshika nafasi 10 za mwisho. Matokeo hayo
ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa
Wastani kwa Kutumia Pointi (GPA) ambao unaonyesha shule zote 10
za kwanza ni za binafsi. Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar
es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), Dk Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni
wanafunzi 196,805 sawa na asilimia 68.33 ya watahiniwa 288,247
waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 235,227, sawa na
asilimia 58.25 ya waliofaulu mwaka 2013. Dk Msonde alisema
wavulana waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na
wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61. Kwa mujibu wa
maelekezo ya BRN, ufaulu wa upande wa sekta ya elimu, ambayo
ilipangiwa malengo tisa, ulipaswa uwe asilimia 70. Hata hivyo,
pamoja na kuwa chini kidogo ( asilimia 1.7) kufikia wastani wa
ufaulu kitaifa, Msonde alisema: “Tumejitahidi kwani ni asilimia
kama moja na ushee ilibaki, walimu walifanya kazi nzuri na nina
imani tutaifikia.” Alisema watahiniwa 297,365 waliandikishwa
kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana 139,400 sawa na asilimia
46.88 na wavulana 157965 sawa na asilimia 53.12. Watahiniwa wa
shule walikuwa 244,902 ikilinganishwa na watahiniwa 367,163
walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka 2013. “Idadi ya
watahiniwa wa shule walioandikishwa kufanya mtihani huo
ilipungua kwa asilimia 33.3 ikilinganishwa na watahiniwa
walioandikishwa mwaka 2013.” “Mwaka 2012 kati ya watahiniwa
386,355 waliofanya mtihani wa kidato cha pili, watahiniwa
136,243 walirudia kidato cha pili na watahiniwa 250,112
waliendelea na kidato cha tatu ambao ndiyo waliosajiliwa kufanya
mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014,” alisema na kuongeza:
“Kati ya watahiniwa 297,365 waliosajiliwa kufanya mtihani wa
kidato cha nne 2014, watahiniwa 288,247 sawa na asilimia 96.93
walifanya mtihani na watahiniwa 9,118 sawa na asilimia 3.07
hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.” Alisema
watahiniwa wa shule, kati ya watahiniwa 244,902 waliosajiliwa
watahiniwa 244,410 sawa na asilimia 98.17 walifanya mtihani
ambao wasichana walikuwa ni 110,603 sawa na asilimia 98.13 na
wavulana ni 129,807 sawa na asilimia 98.19. Watahiniwa 4,492
sawa na asilimia 1.83 hawakufanya mtihani. Kwa upande wa
watahiniwa wa kujitegemea, alisema kati ya watahiniwa 52,463
waliosajiliwa, 47,837 ambao ni sawa na asilimia 91.18, walifanya
mtihani na ambao hawakufanya ni 4,626 sawa na asilimia 8.82.
Ufaulu wa masomo Dk Msonde alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule
katika masomo ya msingi umepanda kati ya asilimia 1.28 na 11.22
ikilinganishwa na mwaka 2013. “Ufaulu wa juu kabisa ni ule wa
somo la Kiswahili na asilimia 69.66 ya watahiniwa wote wa shule
waliofanya somo hili wamefaulu na ufaulu wa chini kabisa ni ule
wa somo la hisabati ambalo asilimia 19.58 ya watahiniwa wote
waliofanya somo hili wamefaulu.” “Ufaulu katika masomo ya
sayansi yaani fizikia, kemia na baiolojia umeendelea kuimarika
kidogo kwa kulingana na ufaulu wa masomo hayo mwaka 2013,”
alisema. Katika matokeo hayo, ufaulu wa kila somo na asilimia
katika mabano ni Kiswahili (69.66), kemia (56.73), Kiingereza
(55.10), baiolojia (48.30), fizikia (46.71), jiografia (37.96),
uraia (37.70), historia (37.41), biashara (34.29), uhasibu
(42.20) na hisabati (19.58). Matokeo yaliyozuiwa, kufutwa Dk
Msonde alisema baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 184
waliobainika kufanya udanganyifu. Kati ya watahiniwa
waliobainika kufanya udanganyifu, 128 ni wa kujitegemea na 56 ni
watahiniwa wa shule. Alisema kati ya watahiniwa hao, 128
wanatoka vituo viwili vya Kisesa mkoani Mwanza na Ubago visiwani
Zanzibar, huku wengine 56 wakitoka shule mbalimbali. “Tumeagiza
mamlaka husika kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika
katika vituo hivyo vya Kisesa na Ubago kwani udanganyifu
uliofanyika ni karatasi moja ya kujibia mtihani imeandikwa na
watu watatu tofauti jambo ambalo linaonyesha hakukuwa na
umakini,” alisema. Shule kongwe na za vipaji hoi Shule za vipaji
kama Ilboru, Mzumbe, Msalato, Kilakala, Tabora Boys, Kibaha na
Tabora Girls na Shule kongwe zinazomilikiwa na Serikali kama
Pugu, Zanaki, Bwiru Boys, Minaki, Azania na Jangwani, kwa mara
nyingine zimeshindwa kufua dafu kwa shule za binafsi. Katika
orodha ya shule 10 bora shule binafsi zilizotamba katika matokeo
hayo ni Kaizirege (Kagera), Mwanza Alliance (Mwanza), Marian
Boys (Pwani), St. Francis Girls (Mbeya), Abbey (Mtwara), Feza
Girls (Dar es Salaam), Canossa (Dar es Salaam), Bethel Sabs
Girls (Iringa), Marian Girls (Pwani) na Feza Boys (Dar es
Salaam). Shule 10 za mwisho ni Manolo (Tanga), Chokocho (Pemba),
Kwaluguru (Tanga), Relini (Dar es Salaam), Mashindei (Tanga),
Njelekela Islamic Seminari (Kigoma), Vudee (Kilimanjaro), Mnazi
(Tanga), Ruhembe (Morogoro) na Magoma (Tanga). Watahiniwa 10
bora kitaifa Dk Msonde aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa kuwa
ni Nyakaho Marungu (Baobab), Elton Jacob (Feza Boys), Samwel
Adam (Marian Boys), Fainess Mwakisimba (St. Francis Girls),
Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys),
Angel Mcharo (St. Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa),
Jenifa Mcharo (St. Francis Girls) na Mahmoud Bakili (Feza Boys).
Wasichana 10 bora kitaifa Katika matokeo hayo mwanafunzi bora
kwa wasichana ni Nyakaho Marungu (Baobab), aliyefuatiwa na
Fainess Mwakisisimba (St. Francis Girls), Angel Mcharo (St.
Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St.
Francis Girls), Levina Ndamugoba (Msalato), Veronica Wambura
(Canossa), Sifaely Mtaita (St Maris Mazinde Juu), Catherine
Ritte (St. Francis Girls) na Anastazia Kabelinde (Kaizerege).
Wavulana 10 bora Dk Msonde alimtangaza kinara kwa wavulana kuwa
ni Elton Jacob (Feza Boys) akifuatiwa na Samwel Adam (Marian
Boys), Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial), Paul Jijimya (Marian
Boys), Mahmoud Bakili (Feza Boys), Amani Andrea (Moshi
Technical), Mahmoud Msangi, Elias Kalembo, Haji Gonga na Kelvin
Sessan wote kutoka Feza Boys. CHANZO MWANANCHI.
*****************************************************
Page 1 of 1