URI:
   DIR Return Create A Forum - Home
       ---------------------------------------------------------
       habari
  HTML https://habari.createaforum.com
       ---------------------------------------------------------
       *****************************************************
   DIR Return to: Jukwaa la elimu Tanzania
       *****************************************************
       #Post#: 3112--------------------------------------------------
       WADAIWA MIKOPO ELIMU YA JUU WAPEWA SIKU 60
   DIR By: stakeholder
       Date: May 5, 2016, 3:14 am
       ---------------------------------------------------------
       Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inatoa siku
       60 kuanzia tarehe 14 Machi, 2016 kwa wanufaika wote wa mikopo
       wanaodaiwa na HESLB kujitokeza na kuanza kulipa madeni yao kabla
       ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
       Aidha, katika muda huu wa siku 60 waajiri pia wanatakiwa
       kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao wa kisheria wa
       kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao waliohitimu katika vyuo vya
       elimu ya juu ndani na nje ya nchi. Taarifa zinazopaswa
       kuwasilishwa zijumuishe majina kamili ya waajiriwa, vyuo na
       mwaka waliohitimu.
       Itakumbukwa kuwa Sheria iliyoanzisha HESLB (Sura 178) (kama
       ilivyorekebishwa) inatoa wajibu kwa mnufaika wa mikopo ya elimu
       ya juu na pia wajibu kwa mwajiri.
       Wajibu wa Mwajiri
       Hivyo basi, taarifa hii inalenga kuwakumbusha waajiri ambao bado
       hawatimizi wajibu wao kisheria (kifungu cha 20) wa kuwasilisha
       majina ya waajiriwa wao wote ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu kwa
       HESLB ndani ya siku 28 tangu waajiriwe. Adhabu ya kutotekeleza
       wajibu huu kwa mwajiri ni faini ya shilingi milioni saba (Tshs
       milioni 7) au kifungo au vyote kwa pamoja.
       Kwa mujibu wa sheria hiyo, baada ya HESLB kupokea orodha kutoka
       kwa mwajiri, itafanya uchambuzi ili kubaini wanufaika wa mikopo
       ya elimu ya juu na kumwelekeza mwajiri kuingiza makato ya
       marejesho kwenye mshahara wa mnufaika na kuwasilisha makato hayo
       kwa HESLB. Adhabu ya kutowasilisha makato kwa HESLB ni faini ya
       asilimia 10 ya makato yote ambayo hayajawasilishwa na faini hii
       inapaswa kulipwa na mwajiri.
       Wajibu wa mnufaika wa mkopo na wazazi, walezi, wadhamini
       Aidha, pamoja na wajibu wa mwajiri kama ulivyofafanuliwa hapo
       juu, wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu tangu mwaka 1994,
       wana wajibu wa kisheria (Kifungu cha 19 cha sheria ya HESLB),
       pamoja na mambo mengine, kuitaarifu HESLB kwa maandishi mahali
       alipo na kuandaa utaratibu wa kulipa deni lake la mkopo wa elimu
       ya juu.
       Iwapo mnufaika wa mkopo atashindwa kutoa taarifa hizo, adhabu
       yake ni kushitakiwa mahakamani.
       Aidha, HESLB inapenda kuwakumbusha wazazi, walezi na wadhamini
       wa wanafunzi walionufaika na mikopo kuwa wana wajibu wa kisheria
       (chini ya kifungu cha 22 cha sheria ya HESLB) wa kuhakikisha
       kuwa taarifa muhimu za mnufaika waliyemdhamini zinaifikia HESLB.
       Kwa mujibu wa kifungu hicho, taarifa hizo ni pamoja na mahali
       alipo mnufaika, majina aliyotumia wakati akipata mkopo, mwajiri
       wake na kuhakikisha mnufaika aliyemdhamini anarejesha mkopo wake
       kwa HESLB.
       
       Iwapo mwajiri, mnufaika au mdau yeyote ana swali, awasiliane na
       HESLB kwa simu zifuatazo: 0754 373481; 0763 459 165 au 022
       2772432/33.
       Lengo la HESLB ni kuhahakisha madeni yote yanakusanywa ili
       kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania wengi zaidi. Ili
       kutekeleza hili, wanufaika, waajiri na wadau wengine wote
       wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kisheria ili HESLB itekeleze
       majukumu yake kama ilivyokusudiwa wakati ilipoanzishwa mwaka
       2004.
       HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na
       kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu
       mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika
       taasisi za elimu ya juu. Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai
       na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za
       elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza
       kukopesha wanafunzi.
       Mwisho
       Imetolewa na:
       Bw. Jerry Sabi,
       Kaimu Mkurugenzi Mtendaji – HESLB
       Dar es Salaam – Jumapili, Machi 13, 2016
       sorce:
  HTML http://www.heslb.go.tz/index.php/application-guidelines/198-wadaiwa-mikopo-elimu-ya-juu-wapewa-siku-60
       *****************************************************
       Page 1 of 1