URI:
   DIR Return Create A Forum - Home
       ---------------------------------------------------------
       habari
  HTML https://habari.createaforum.com
       ---------------------------------------------------------
       *****************************************************
   DIR Return to: Makala Bora
       *****************************************************
       #Post#: 2454--------------------------------------------------
       Magufuli afuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo
   DIR By: Wilson John
       Date: November 7, 2015, 9:24 am
       ---------------------------------------------------------
       Dar es Salaam.Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John
       Pombe Magufuli amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo
       hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa.
       Dk Magufuli ameagiza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya
       nchi zifanywe na kusimamiwa  na mabalozi wanaoiwakilisha
       Tanzania nchi za nje.
       Uamuzi huo wa rais ameutoa Ikulu jijini Dar es Salaam katika
       kikao kilichojumuisha watendaji mbalimbali wa serikali wakiwemo
       Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu na
       Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
       Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari ruhusa ya
       safari nje ya nchi inaweza kutolewa kwa jambo la dharura ambalo
       hata hivyo jambo hilo lazima lipate kibali cha Katibu Mkuu
       Kiongozi.
       ˇ°Badala yake rais ametaka ziara nyingi zielekezwe kwenda
       vijijini ili kuwawezesha watendaji kujua na kutatua kero za
       wananchiˇ± imesema taarifa hiyo.
       Katika kikao hicho, rais ameelekeza pia mambo kadhaa ambayo
       watendaji hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na
       kuyapanga vizuri ili yasimamiwe mara moja na Baraza la Mawaziri
       atakaloliteua.
       Mambo hayo ni pamoja na kuanza kwa mikakati ya kuhakikisha
       wanafunzi wote wanaanza kupatiwa elimu ya bure kuanzia Januari
       mwakani.
       Taarifa hiyo imetaja jambo la pili kuwa ni suala la uratibu wa
       mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo ameagiza lifanyiwe
       kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri
       zaidi.
       Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rais amemuagiza Kamishna wa TRA
       kusimamia kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato na
       kuhakikisha kero ndogo ndogo zinazowakabili wananchi zinaanza
       kushughulikiwa mara moja.
       Ameitaka TRA kukusanya mapato toka kwa wafanya biashara wakubwa
       na wakwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote na
       kusisitiza kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kubatilisha maamuzi
       hayo zaidi yake.
       Dk Magufuli ametaka usimamizi mzuri katika suala la manunuzi ya
       umma ambalo amesema limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa
       maofisa wasio waaminifu kuiibia serikali kwa kuongeza bei za
       bidhaa na huduma tofauti na bei halisi ya manunuzi.
       *****************************************************
       Page 1 of 1